Serikali inaimarisha juhudi zake za kuboresha miundombinu ya dijitali, ili kupanua uunganishaji, kuchochea uchumi wa dijitali na kufanikisha ukuaji wa uchumi.
Katibu wa Utangazaji na Mawasiliano Stephen Isaboke, amesema miundombinu ya dijitali sio tu swala la kiteknolojia, lakini msingi muhimu kwa uchumi na utoaji wa huduma muhimu.
Akizungumza alipofungua makala ya nne ya kongamano la ITW na Datacloud Africa Jijini Nairobi, Isaboke alitoa wito wa kuangaziwa zaidi kwa usalama, utegemeaji na uthabiti wa miundombinu hiyo, akitaja ukuaji wa uchumi wa dijitali Afrika.
“Miundombinu ya dijitali ni msingi wa uchumi wetu na utoaji wa huduma muhimu, na inapokosa kufaulu, huathiri maisha na imani ya umma,” alisema Isaboke.
Isaboke alisema upanuzi wa miundombinu ya Kenya unapaswa kuambatana na mikakati ya kuhakikisha mifumo ya dijitali inauwezo wa kustahimili changamoto za kiteknolojia na zile za kimazingira.
Kongamano hilo linajiri huku mataifa ya Afrika yakilenga kuimarisha ushiriki wao katika uchumi wa kidijitali duniani na kunufaika na huduma za dijitali zinazoendelea kupanuka.