Rais William Ruto leo Jumatano, ameanza ziara rasmi ya siku nne katika eneo la South Rift.
Kwenye ziara hiyo, kiongozi wa taifa anatarajiwa kukagua na kuzindua miradi kadhaa ya maendeleo katika kaunti za Bomet na Kericho.
Miongoni mwa miradi ambayo anatarajiwa kukagua ni pamoja na ujenzi wa uwanja mdogo wa ndege wa Itembe, hospitali ya mama na mtoto ya Bomet na ujenzi wa barabara Bomet mjini.
Miradi mingine atakayokagua ni ujenzi wa uwanja wa Kapkatet, shule ya msingi ya Rungut,huku akitarajiwa kuwahutubia wananchi katika maeneo tofauti ya South Rift.
Ziara hii ya South Rift inajiri baada ya ziara ya kufana katika kaunti ya Kajiado juma lililopita.