Miano atoa wito wa kulindwa kwa ndege wa kuhamahama

Waziri amesema hatua ya Kenya ya kuwa na maeneo mengi yaliyolindwa, yanaifanya kuwa kitovu cha uhifadhi wa ndege na wanyamapori wengine.

Tom Mathinji
2 Min Read
Rebecca Miano - Waziri wa Utalii na Wanyamapori.

Waziri wa Utalii na Wanyamapori Rebecca Miano ametoa wito wa ushirikiano wa kimataifa katika kuwalinda ndege wa kuhamahama.

Wito wa Waziri Miano unajiri huku taifa hili likiwa mwenyeji wa zaidi ya mashirika 120 ya uhifadhi kutoka kote duniani kwenye mkutano wa kimataifa wa shirika la BirdLife na kongamano la Flyways Summit 2026.

Mkutano huo unaofanyika jijini Nairobi umewaleta pamoja wahifadhi na viongozi kutoka Afrika, Asia, Marekani, Ulaya, Mashariki ya Kati na Pasifiki ili kujadili ulinzi wa ndege wa kuhamahama na makazi yao.

Miano alisema mkutano huo unatoa fursa kwa mataifa na mashirika ya uhifadhi kushirikisha juhudi zao na kukusanya rasilimali ili kuwalinda ndege hao.

Kulingana na Waziri huyo, ushiriki wa viongozi hao ni muhimu katika kuwahusisha na sera za kimataifa kuhusu uhifadhi, kwa kuzingatia utafiti wa kisayansi na juhudi za kijamii.

Aidha, alidokeza kuwa hatua ya Kenya ya kuwa na maeneo mengi yaliyolindwa, yanaifanya kuwa kitovu cha uhifadhi wa ndege na wanyamapori wengine.

Alisema Kenya ni nyumbani kwa zaidi ya aina 1,100 za ndege , wakiwemo wale wa humu nchini na wa kuhamahama ambao hutegemea makao katika anga ya kimataifa.

Waziri huyo alielezea mipango ya serikali ya uhifadhi, ikiwa ni pamoja na uhifadhi wa hekari 130,000 wa eneo la Mto Tana, upanzi wa miti Mlima Kenya na juhudi za kulinda ndege aina ya Tai katika maeneo ya Maasai Mara na Amboseli.

Wakati huo huo Miano alimkaribisha Binti Mfalme Takamado wa Japani, ambaye ni Rais wa Shirika la BirdLife International, anayehudhuria kongamano hilo.

Wengine wanaohudhuria ni pamoja na mwenyekiti wa BirdLife International Dkt. Mike Rands, Afisa Mkuu Mtendaji Martin Harper na Afisa Mkuu wa Nature Kenya, Dkt. Paul Matiku.

TAGGED:
Share This Article