Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zubeir bin Ally, amefafanua kuhusu suala ambalo limekuwa likiwasumbua wengi kuhusu masharti ya eda.
Mjadala kuhusu kipindi hicho cha mapumziko kwa mwanamke wa Kiisilamu aliyefiwa na mumewe au kutalikiwa, ulitokana na kifo cha hivi punde cha mume wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
Kulingana na Sheikh Zubeir, sheria ya Kiislamu haimzuii mwanamke aliyefiwa na mumewe kuendelea na shughuli au majukumu muhimu yanayomhitaji yeye mwenyewe wakati akiwa katika kipindi cha eda.
Amesema hilo linawezekana iwapo hakuna mtu mwingine anayeweza kutekeleza majukumu hayo kwa niaba yake, huku mwanamke huyo akizingatia masharti na taratibu zilizowekwa na Sheria ya Kiislamu kuhusu kipindi cha eda.
Akitoa mfano wa Rais Samia, ambaye amefiwa na mumewe, Sheikh Zubeir amesema Rais anaweza kuendelea kutekeleza majukumu ya kitaifa ambayo yanamhitaji yeye mwenyewe.
Alikuwa akizungumza leo, Jumatano, Septemba 9, 2026, katika Makao Makuu ya Baraza la Waislamu Tanzania katika mkutano na wanahabari.