Maandalizi ya sherehe za mwaka huu za Sikukuu ya Mashujaa yamezidi kushika kasi, huku kaunti za Elgeyo Marakwet, Nandi na Uasin Gishu zikitarajiwa kuandaa hafla hiyo ya kitaifa kwa pamoja.
Waziri wa Usalama wa Kitaifa Kipchumba Murkomen amesema maandalizi hayo yanaendelea vizuri baada ya kuanza ziara ya kukagua miradi inayohusishwa na sherehe hizo katika kaunti hizo tatu.
Murkomen alianza ziara yake ya ukaguzi katika Uwanja wa Kamariny, Kaunti Ndogo ya Keiyo Kaskazini, ambapo ujenzi umekamilika kwa kiwango cha zaidi ya nusu.
Uwanja huo unatarajiwa kuandaa shughuli za michezo za kabla ya sherehe hizo.
Alisema miradi mingine, ikiwemo barabara, maji, nishati na miundombinu ya umeme, pia inaendelea. Makao makuu mapya ya kaunti yanajengwa katika mji wa Iten kama sehemu ya juhudi za kuboresha miundombinu ya umma.
Mashindano ya michezo pia yatafanyika Tot, huko Kerio Valley, kuadhimisha kurejea kwa amani katika eneo hilo.
Kaunti ya Nandi itaandaa mkutano wa kitaifa wa vijana, huku mkutano wa michezo na mashindano ya kitamaduni yakiwa miongoni mwa shughuli zitakazofanyika kuelekea Siku ya Mashujaa.
Ukaguzi huo ulihusisha maafisa wakuu wa serikali na viongozi wa eneo hilo, wakiwemo Magavana Wisley Rotich na Jonathan Bii, Mbunge wa Keiyo Kaskazini Adams Kipsanai na Kamishna wa Kanda ya Bonde la Ufa Abdi Hassan.
Murkomen alisema miradi inayoendelea ni muhimu katika kuhakikisha eneo hilo liko tayari kuandaa sherehe hizo za kihistoria.