Mwanamuziki wa Uganda Vinka ameahidi mashabiki wake tamasha ya kipekee anapokamilisha maandalizi ya tamasha yake ya kwanza.
Mrembo huyo ambaye yuko chini ya usimamizi wa kampuni ya na Swangz Avenue anaandaa tamasha ya “Vinka Live and Loud”, leo Ijumaa Agosti 21, 2026 katika uwanja wa Lugogo jijini Kampala.
Vinka na usimamizi wake walikamilisha maandalizi ya onyesho hilo la leo ambalo limekuwa likisubiriwa kwa muda mrefu, huku mashabiki wakihimizwa kufika mapema kwa ajili ya usiku wa muziki, maonyesho na mambo mengi mazuri.
Walihutubia wanahabari katika uwanja Lugogo jana ambapo waliahidi kugeuza mkusanyiko wa nyimbo zake za miaka yote ya muziki kuwa onyesho bora la moja kwa moja.
Tamasha hiyo ni onyesho la safari ya Vinka kutoka kuwa mcheza densi wa ziada hadi kuwa mmoja wa wasanii wakuu nchini Uganda.
“Tamasha hii ni heshima kwa kila mtu ambaye amekuwa akicheza, kuimba na kusimama nami tangu siku ya kwanza,” alisema mrembo huyo.
Nakiyingi Veronica Lugya, au ukipenda Vinka ni mwimbaji, mtunzi wa nyimbo na mcheza densi maarufu kutoka Uganda, aliyezaliwa tarehe 27 Juni 1994.
Alianza kazi yake kama mcheza densi wa kitaalamu na meneja wa wasanii kabla ya kuanza rasmi safari yake ya muziki mwaka 2017.
Ana mikataba ya usimamizi na kampuni ya Swangz Avenue nchini Uganda na kampuni ya kimataifa ya Sony Music Entertainment.