Naibu Rais Kithure Kindiki amesema serikali ya kitaifa iko kwenye mwelekeo sahihi katika kutekeleza mipango ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya Wakenya.
Kwa mujibu wa Kindiki, United Democratic Alliance, UDA ndicho chama pekee cha kisiasa nchini Kenya chenye maafisa waliochaguliwa katika kila kituo cha kupigia kura nchini.
Amesema maafisa 20 wa UDA katika kila kituo cha kupigia kura watakuwa kikosi cha chama mashinani.
Watu hao kulingana naye, wana jukumu la kueleza maendeleo ya serikali katika kutekeleza manifesto ambayo serikali ya Kenya Kwanza ilichaguliwa nayo Agosti mwaka 2022.
Kwa mujibu wa Naibu Rais, maafisa hao watakuwa mstari wa mbele kueleza juhudi za serikali za kuimarisha uchumi, kubadilisha uzalishaji wa kilimo, kuboresha elimu na huduma za afya, kuunda nafasi za ajira, pamoja na kupanua usambazaji wa umeme vijijini na miundombinu ya michezo.
Kindiki amesema maafisa hao wa ngazi ya mashinani pia watakuwa na jukumu muhimu la kutetea rekodi ya serikali dhidi ya vyama vya kisiasa ambavyo, kulingana naye, vinatafuta uongozi kupitia kile alichokiita uongo, kelele zisizo za msingi na kaulimbiu zisizo na maana.
Alisema hayo baada ya kukutana na maafisa 15,000 wa UDA wa ngazi ya mashinani kutoka maeneo mbalimbali ya kaunti ya Tharaka Nithi, nyumbani kwake Irundune.
Aliwapongeza kwa kuchaguliwa kwao na kuwaagiza kukitetea chama pamoja na serikali huku nchi ikiingia katika mwaka wa uchaguzi.
Pia aliwasihi Wakenya kumuunga mkono Rais William Ruto katika azma yake ya kuchaguliwa tena.