Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) imewaonya wanasiasa dhidi ya kutoa semi za chuki na kusababisha migawanyiko ya kikabila nchini, ikisema itawachukulia hatua wanaohujumu mshikamano wa taifa.
Akizungumza na wanahabari, mwenyekiti wa NCIC Kasisi Dkt. Kepha Nyamweya Omae alielezea wasiwasi kutokana na kile alichokitaja kuwa ongezeko la uhasama wa kisiasa, huku taifa linapojiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
“Katika muda wa miezi michache iliyopita, tumeshuhudia ongezeko la semi za chuki za kisiasa. Kama tume, tumesikitishwa na ubaguzi wa kikabila na matamshi ambayo yanaweza kusababisha uhasama miongoni mwa jamii,” alisema Omae.
Kulingana na mwenyekiti huyo, semi za chuki na ubaguzi wa kikabila ni tisho kubwa kwa uthabiti wa demokrasia wa taifa hili.
“Tunatoa wito kwa wanasiasa wote, bila kuzingatie miegemeo yao ya kisiasa, kuvumiliana wakati wa shughuli zao kwa umma.”