Wakazi wa Nairobi sasa watanufaika na huduma za mahakama karibu na makazi na maeneo yao ya biashara na kazi kufuatia kuzinduliwa kwa Mahakama Tamba na Idara ya Mahakama.
Mahakama hiyo iliyo kwenye gari, inalenga kuharakisha utatuzi wa migogoro ya madai madogo.
Jaji Mkuu Martha Koome alizindua rasmi Mahakama hiyo siku chache zilizopita, katika uwanja wa Mahakama ya Upeo, hafla iliyohudhuriwa na Naibu Rais Kithure Kindiki.
Mpango huo unalenga kukabiliana na changamoto zinazotokana na kutosambazwa kwa usawa kwa vituo vya mahakama katika Kaunti ya Nairobi.
Haya yanajiri huku kukiwa na jumla ya kesi 92,295 zinazosubiri kusikilizwa au zinazoendelea kushughulikiwa Nairobi, na ni kaunti ndogo saba pekee kati ya 17 zilizo na mahakama.
Mahakama Tamba itahudumu katika masoko, vituo vya biashara na maeneo ambayo hayana huduma za kutosha za mahakama, ikilenga biashara ndogo na watu binafsi wanaokumbwa na changamoto za kufika katika mahakama za kawaida.
Maeneo yatakayoanza kunufaika ni pamoja na Gikomba, Toi, Kawangware, Githurai 45, Kangemi, Kamukunji, Kibra, Dagoretti North, Kasarani/Roysambu na Westlands.
Mpango huo unatarajiwa kupunguza gharama za usafiri na muda wa kufika mahakamani, kupunguza msongamano katika vituo vyenye shughuli nyingi, hususan Mahakama za Biashara za Milimani na Makadara na kuharakisha utatuzi wa kesi zinazostahili kusikilizwa chini ya utaratibu wa madai madogo.