Serikali yaimarisha msako dhidi ya majangili Isiolo

Muganda alisema maafisa zaidi wa akiba kutoka eneo la Gotu, wataajiriwa na kupewa silaha kuimarisha hali ya usalama katika eneo hilo.

Tom Mathinji
1 Min Read
Serikali yaimarisha msako dhidi ya majangili Isiolo.

Mrakibu wa Mashariki mwa nchi Jacob Muganda, amesema serikali imechukua hatua madhubuti kurejesha hali ya utulivu katika eneo la Gotu na maeneo jirani katika kaunti ya Isiolo, kufuatia mashambulizi ya majangili yaliyosababisha vifo vya watu watano.

Miongoni mwa waliofariki ni pamoja na maafisa wawili wa polisi kutoka kitengo cha kukabiliana na wezi wa mifugo (ASTU), afisa mmoja wa akiba na raia wawili.

Akizungumza mjini Isiolo baada ya kuongoza kundi la maafisa wa usalama kuzuru maeneo yaliyoathiriwa, Muganda alithibitisha kuwa serikali imewapeleka maafisa zaidi wa usalama, imeimarisha doria na kutoa magari ya kivita kufanikisha usalama wa maafisa wa polisi wanapokabiliana na visa vya utovu wa usalama.

Kulingana na mrakibu huyo, maafisa zaidi wa akiba kutoka eneo la Gotu, wataajiriwa na kupewa silaha kuimarisha hali ya usalama katika eneo hilo.

Muganda aliwahimiza wakazi wa Gotu na maeneo jirania kurejelea shughuli zao za kawaida bila wasiwasi.

Aidha, alidokeza kuwa maafisa wa upelelezi wanafuatilia habari muhimu kutoka kwa simu za mkononi na vifaa vingine zilizoachwa kwenye eneo la mkasa.

Share This Article