Mechi za msimu mpya wa Ligi Kuu ya Soka hapa nchini (FKF), zilizotarajiwa kuanza leo Jumamosi, zimeahirishwa.
Kupitia kwa taarifa, Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), limesema limeahirisha mechi hizo kwa muda usio julikana, likidokeza kuwa litatoa habari kamili baadaye kuhusu hatua hiyo.
“Tunasikitika kufahamisha vilabu na washirika husika kwamba mwanzo wa msimu mpya wa ligi umeahirishwa kwa muda usiojulikana,” ilisema FKF.
Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Gor Mahia wanalitarajiwa kutetea taji lao dhidi ya Murang’a Seal katika uwanja wa michezo wa taifa wa Nyayo, huku Ulinzi Stars ilitarajiwa kuwa mwenyeji wa Tusker FC, nayo Mathare United ingeikaribisha APS Bomet katika Uwanja wa Kasarani Annex Jijini Nairobi.
Katika kaunti ya Kirinyaga, Posta Rangers ilitarajiwa kumenyana na Shabana katika Uwanja wa Wang’uru mechi ambayo iingepeperushwa moja kwa moja kwenye runinga ya KBC Channel 1 kuanzia saa tisa alasiri.
Timu ya Gor Mahia imewahimiza mashabiki wake waliokuwa wamenunua tiketi kutokuwa na wasiwasi, kwani watazitumia mechi hicho zitakaporejelewa.