Viongozi wa upinzani wamwomboleza babake Martha Karua

Wanaombea familia faraja katika kipindi hiki kigumu na kumuomba Mungu ailaze roho ya Mwalimu Jackson Karua mahali pema.

Marion Bosire
1 Min Read

Viongozi wa upinzani nchini Kenya wametuma salamu za pole kwa Waziri wa zamani wa Sheria, Martha Karua, kufuatia kifo cha babake, Mwalimu Jackson Karua.

Seneta wa zamani wa Baringo, Gideon K. Moi, alimtaja Martha Karua kuwa dadake mkubwa na akatuma pole kwa familia nzima ya Karua.

Alisema ingawa hakupata fursa ya kumfahamu Mzee Jackson binafsi, maadili yake ya uadilifu, ukweli na nidhamu vinaonekana wazi kupitia watoto aliowalea.

Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, alieleza masikitiko makubwa kufuatia kifo hicho, akimtaja Mwalimu Karua kama baba mpendwa wa Martha.

Alitoa pole kwa familia na kuwaombea wapate nguvu, akirejelea kifungu cha Biblia, Zaburi 34:18, isemacho Mungu yu karibu na waliovunjika moyo.

Kiongozi wa chama cha DAP-K, Eugene L. Wamalwa, alisema amesikitishwa sana na msiba huo na kumwombea Karua na familia yake nguvu, amani na faraja katika kipindi hiki cha maombolezo.

Gavana wa kaunti ya Siaya, James Orengo, pia aliomboleza kifo cha Mwalimu Jackson Karua, akituma salamu za rambirambi kwa Martha, familia ya Karua na wote waliomfahamu.

Viongozi hao waliiombea familia faraja katika kipindi hiki kigumu na kumuomba Mungu ailaze roho ya Mwalimu Jackson Karua mahali pema.

Share This Article