Maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), wamemkamata afisa wa Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru (KRA), kwa madai ya kuitisha na kupokea hongo.
Kulingana na EACC, afisa huyo aliitisha fedha ili afanikishe utoaji wa cheti cha kuthibitisha ulipaji ushuru kwa kampuni moja ya ujenzi.
Mshukiwa huyo Hughes Obilo, afisa katika Idara ya Urejeshaji Madeni mjini Kisumu, anadaiwa aliitisha shilingi 100,000 kutoka kwa kampuni hiyo ya ujenzi, ili afutilie mbali deni la ushuru linalodaiwa kampuni hiyo la shilingi milioni 4.5, kutoka kwa mfumo wa ulipaji ushuru wa iTax.
Baada ya kutekeleza uchunguzi wa awali, EACC ilitekeleza operesheni iliyosababisha kukamatwa kwa mshukiwa huyo akipokea shilingi 30,000.
Mshukiwa huyo alikamatwa Septemba 14, 2026 mjini Kisumu na anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Central, mjini Kisumu.
“EACC imejitolea kukabiliana na ulaji rushwa na ufisadi katika afisi za umma, na itachukua hatua kali kwa wale wanatumia vibaya afisi hizo,” ilisema EACC kupitia kwa taarifa.