Tibaijuka ashauri Lissu aachiliwe

Anamshauri Rais Samia kutumia hekima iliyomwongoza kutangaza sera ya 4Rs kumwachia huru Lissu kwa sababu kesi haikamiliki.

Marion Bosire
2 Min Read
Kiongozi wa chama cha CHADEMA Tundu Lissu

Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi nchini Tanzania Profesa Anna Tibaijuka, sasa anashauri kwamba mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu aachiliwe huru.

Tibaijuka anamshauri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kutumia hekima iliyomwongoza kutangaza sera ya 4Rs kumwachia huru Lissu kwa sababu kesi haikamiliki.

Kupitia ukurasa wake wa X, jana Julai 13, 2026 Tibaijuka aliandika, “Dkt. Samia Suluhu, Mhe Rais naendelea kushauri kwa dhati Tundu Lissu aachiwe huru kwani kesi haikamiliki, hekima na busara iliyokufanya kutangaza sera ya 4Rs mara ulipoingia madarakani ikuongoze tena katika jambo hili”

Kulingana na Tibaijuka simulizi za kutisha za vyombo vya habari vya kimataifa kuhusu kesi ya Lissu, zinaibua hisia kali hasa kwa Vijana.

Alitaja pia wazee akisema, “Tumekumbushwa kadhia ya operation Sogeza iliyounda Vijiji vya ujamaa 1974 -1976, taarifa hizi zinaathiri kikubwa taswira ya Taifa letu na maslahi yake, athari ni kubwa.”

Mama huyo ambaye amewahi kufanya kazi Nairobi katika afisi za Umoja wa Mataifa, anataka uongozi wa Tanzania utafute muafaka kupitia uwajibikaji na maridhiano.

“Tuwe na hofu ya Mungu na kutambua miujiza yake mfano wa risasi 16 kushindwa kukomesha uhai ingawa maumivu ni makubwa, tutubu na kusali kuliombea Taifa letu kila Mtu kwa imani yake,” alimalizia Tibaijuka.

Tundu Lissu anakabiliwa na kesi ya uhaini ambayo imekuwa ikijikokota.

Share This Article