Gavana wa zamani wa kaunti ya Taita Taveta Mhandisi John Mruttu ameanzisha hatua za kusuluhisha matatizo yanayohusiana na umiliki wa ardhi nchini Kenya.
Katika kile anachokitaja kuwa hatua muhimu kuelekea kwa haki kwa wananchi, Mrutu aliwasilisha rasmi ombi la marekebisho ya sheria za ardhi ya Kiasili na urithi kwa Spika wa Bunge la Taifa, Moses Wetang’ula jana.
“Hii ni hatua ya kwanza na muhimu sana katika safari ya kurekebisha dhuluma ambayo imeathiri familia nyingi za Wakenya kwa miaka mingi” alisema Mruttu.
Mhandisi huyo ambaye kwa sasa anahudumu kama mwenyekiti wa shirika la ufadhili wa kilimo nchini AFC, amesema pia kwamba tayari ya kutajwa kwa mjadala tayari imepangwa na “mchakato umeanza rasmi”.
Kulingana naye wajane, mayatima na vijana wamekuwa wakiteseka muda mrefu chini ya mfumo mgumu wa kisheria, wakishindwa kumiliki, kutumia au kuendeleza ardhi ambayo ni haki yao, kwa sababu taratibu za urithi ni ghali, ngumu na huchukua muda mrefu sana.
Anaamini kwamba hali hiyo itabadilika na kutakuwa na Kenya ambapo mjane hatalazimika kupitia misukosuko ya kisheria ili kupata haki ya makazi yake, yatima hatanyimwa urithi wake na Kijana ataweza kutumia ardhi ya kurithi kujenga maisha yake.
“Tunafanya kazi kuelekea mfumo ambapo umiliki wa ardhi ya kurithi unakuwa rahisi, wenye heshima na unaofikiwa na wote, bila kulazimika kupeleka kila jambo Mahakama Kuu” alisema Mhandisi Mruttu.