Shirika la Utabiri wa hali ya Hewa (KMSA), limesema hali ya mawingu inayoshuhudiwa katika baadhi ya sehemu za nchi ikiwa ni pamoja na Nairobi, imesababishwa na mfumo wa hali ya hewa unaojulikana Madden-Julian Oscillation (MJO).
Afisa Mkuu wa shirika hilo Jemimah Gacheru, alisema MJO kwa sasa iko katika awamu mbili, ya kwanza na ya pili ambayo imehusishwa na ongezeko la mvua katika sehemu za nchi.
Kulingana na Gacheru, mabadiliko ya hali ya anga kutoka kwa msimu wa baridi hadi ule wa mvua za Oktoba-Noevemba-Disemba, huenda yakasababisha hali ya baridi katika kanda hii.
Katika utabiri wa hali ya hewa juma hili, shirika hilo limedokeza kuwa mvua inatarajiwa katika kaunti za Baringo, Bomet, Bungoma, Busia, Elgeyo/Marakwet, Embu, Garissa, Homa Bay, Kajiado, Kakamega, Kericho, Kiambu, Kilifi, Kirinyaga, Kisii, Kisumu, Kitui, Kwale,na Laikipia.
Kaunti zingine ambazo pia zitashuhudia mvua ni pamoja na Lamu, Machakos, Makueni, Mandera, Marsabit, Meru, Migori, Mombasa, Murang’a, Nairobi, Nakuru, Nandi, Narok, Nyamira, Nyandarua, Nyeri, Siaya, Taita/Taveta, Tana River, Tharaka-Nithi, Trans Nzoia, Uasin Gishu, Vihiga, Wajir na Pokot Magharibi.
Kwenye utabiri huo, shirika hilo limesema viwango vya joto vinatarajiwa kuwa chini ya nyuzijoto 10 katika kaunti za Meru, Tharaka Nithi, Kirinyaga, Murang’a, Nyeri, Nakuru, Narok, Taita/Taveta na Kajiado.
Aidha, nyakati za mchana viwango vya joto vinatarajiwa kuwa zaidi ya nyuzijoto 30 katika kaunti za Kilifi, Tana River, Lamu, Garissa, Wajir, Isiolo, Marsabit na Turkana.