Kagombe agura chama cha UDA

Alilaumu utawala wa Rais William Ruto kwa kushindwa kutimiza ahadi muhimu za kampeni walizopatiwa wakazi wa Gatundu Kusini.

Marion Bosire
2 Min Read

Mbunge wa Gatundu Kusini, Gabriel Kagombe, ametangaza uamuzi wake wa kukatiza uhusiano wake na chama cha United Democratic Alliance, UDA.

Akihutubia umati katika hafla ya mazishi katika kijiji cha Karangi, Gatundu Kusini kaunti ya Kiambu, Kagombe alilaumu utawala wa Rais William Ruto kwa kushindwa kutimiza ahadi muhimu za kampeni walizopatiwa wakazi wa Gatundu Kusini.

Kagombe, aliyechaguliwa kwa tiketi ya UDA mwaka 2022, alisema hawezi tena kuendelea kuunga mkono serikali ambayo, kwa maoni yake, imeshindwa kuleta maendeleo yenye maana kwa wananchi wake licha ya kupata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwao.

Kagombe alitaja barabara za Mau Mau ambazo zimesimama kama mojawapo ya kasoro kubwa za serikali katika eneo hilo, akisema barabara hizo zimeendelea kuwa katika hali mbaya kwa zaidi ya miaka minne.

Hali hiyo alisema imeathiri pakubwa shughuli za kiuchumi katika eneo hilo, hasa wakulima ambao wanatatizika kusafirisha mazao yao hadi sokoni.

Kagombe, ambaye pia ni mkurugenzi wa Kanda ya Kwanza katika Mamlaka ya Maendeleo ya Majani Chai, KTDA, aliikosoa serikali pia kwa kile alichokiita kushindwa kutekeleza kiwango cha Mapato ya Chini Yanayohakikishwa, GMR ambacho wakulima waliahidiwa.

Alipinga kile alichokitaja kuwa ni kuongezeka kwa mzigo wa kifedha kwa wakulima wa chai, hasa ushuru uliopendekezwa na ule uliopo unaoathiri sekta ya chai.

Share This Article