Juhudi za uokoaji zaendelea Columbia

Tetemeko la ardhi limesababisha vifo vya watu 254 kote nchini humo, wengi wakiwa katika miji ya Pereira na Cali.

Marion Bosire
1 Min Read

Siku moja baada ya tetemeko la ardhi la ukubwa wa 7.4 kutikisa magharibi mwa Colombia, waokoaji wanahangaika kuchimba kwenye vifusi vya majengo yaliyoporomoka ili kuwapata manusura na kuopoa miili.

Tetemeko hilo lenye nguvu limesababisha vifo vya angalau watu 254 kote nchini humo, wengi wao wakiwa katika miji ya Pereira na Cali, kulingana na takwimu za serikali.

Takriban nyumba 5,000 ziliharibiwa, kwa mujibu wa Afisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu, huku majengo kadhaa, mengi yakiwa ya makazi, yakianguka kabisa.

Huko Cali, jiji la tatu kwa ukubwa nchini Colombia, angalau watu 95 wamefariki, na majengo 45 yameanguka kabisa au kwa sehemu, kulingana na takwimu za serikali ya eneo hilo.

Juhudi za uokoaji zinaendelea katika Jengo la Vanessa, kusini mwa jiji. Jengo hilo la makazi lenye ghorofa saba liligeuka kuwa kifusi baada ya tetemeko la ardhi la Jumatatu.

Waokoaji sasa wanatumia nyundo, koleo na mashine nzito katika juhudi za kupenya tabaka nene za zege na kuwaokoa takriban watu 20 wanaokadiriwa kunaswa chini ya vifusi.

Jengo hilo lilipoanguka liliangukia jengo lililokuwa kando, ambalo lilikuwa na kituo cha kulelea watoto, ambapo takriban watoto 17 wamenaswa chini ya vifusi.

Kituo hicho kilikuwa sehemu ya Kanisa la Waadventista lililokuwa karibu.

Share This Article