Ugomvi wa Nandy na Zuchu: Yammi aibuka na mazito

Anasema akiwa chini ya usimamizi wa Nandy, Nandy aliwahi kumshauri amteke Diamond.

Marion Bosire
2 Min Read
Yammi Tz

Ugomvi kati ya wanamuziki wawili nyota wa kike nchini Tanzania Nandy na Zuchu unaendelea kupamba moto huku mwanamuziki chipukizi Yammi akizua mazito kuhusu Nandy.

Yammi ambaye jina lake halisi ni Yasirun Yasin Shaban, aliwahi kuwa chini ya usimamizi wa kampuni ya Nandy ya kusimamia wanamuziki ya The African Princess.

Nandy alimtambulisha Yammi kwa mara ya kwanza Januari 2023 kama msanii wa kwanza kuwahi kusajiliwa chini ya kampuni yake lakini hakukaa huko sana.

Mei 5, 2025, Yammi alitangaza kwamba amegura kampuni ya Nandy na kuwa msanii huru, wakati huo akielezea kwamba ametoka kwa uzuri lakini muda mfupi baadaye akadai kwamba ameitishwa shilingi milioni 100 za Tanzania sawa na shilingi milioni 4.8 za Kenya kabla ya kuruhusiwa kuondoka.

Sasa sauti ya mrembo huyo ilichapishwa kwenye Insta Stories na Zuchu, ambapo anasikika akisema kwamba akiwa chini ya usimamizi wa Nandy, Nandy aliwahi kumshauri amteke Diamond kimapenzi.

Katika sauti hiyo iliyonakiliwa, Yammi anasikika akidai kwamba Nandy alimtaka awe kwenye uhusiano wa kimapenzi na Diamond Platnumz aliyekuwa mpenzi wa Zuchu na akubali hata kuwa na mtoto wake kama njia ya kudhalilisha Zuchu.

Lakini huenda ugomvi huu ukawa kiki tu za kutangaza ujio wa albamu ya Nandy ya 911 atakayozindua rasmi Novemba 27, 2026.

Share This Article