Mama Taifa Bi. Rachel Ruto, leo ameongoza sherehe ya kuadhimisha miaka 17 ya uwepo wa shirika aliloasisi la Joyful Women, katika Ikulu ya Nairobi.
Mkewe Rais alidhihirisha furaha ya kipekee kupitia mitandao ya kijamii ambapo alichapisha picha za tukio la leo akisema, “Miaka 17 ya wema, neema na uaminifu wa Mungu! Tumefurahi kuikaribisha familia ya Joyful Women katika Ikulu ya Nairobi tulipoadhimisha safari hii ya kipekee ya uwezeshaji, ustahimilivu na mshikamano wa kindugu miongoni mwa wanawake”.
Alisema kwamba wazo hilo lilianza kama maono lakini limekua na kuwa vuguvugu linalobadilisha maisha kupitia mfumo wa kuweka na kukopeshana fedha, ujumuishaji wa kifedha, ukuzaji wa ujuzi na ujasiriamali.
Bi. Rachel Ruto aliongeza kusema kwamba kufikia sasa, shirika la Joyful Women limezungusha zaidi ya Shilingi bilioni 4 za Kenya, na hivyo kuwawezesha wanawake kuboresha maisha yao na kujenga familia imara zaidi.
Maadhimisho hayo pia yalitoa fursa ya kuzindua nchini Kenya kampeni ya Shirika la Wake za Marais kwa Ajili ya Maendeleo, OAFLAD, ya mwaka 2025–2027.
Kampeni hiyo inaitwa “Kujenga Ustahimilivu wa Kina Mama na Wasichana Katika Mabadiliko ya Tabianchi na Migogoro”.
Inalenga kujenga ustahimilivu wa wanawake na wasichana wanapokabiliwa na mabadiliko ya tabianchi na migogoro na inatambua wanawake kama wadau muhimu katika hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kujenga ustahimilivu wa jamii.
“Tunatoa shukrani za dhati kwa kila mwanamke, mshirika na mfuasi aliyekuwa sehemu ya safari hii. Tuendelee kusaidiana, kuwezeshana na kuunda fursa kwa vizazi vijavyo” alihimiza Mama Taifa Rachel Ruto akimalizia na kauli hii, “Twasherehekea Hatua Zetu!”