Waziri wa Mambo ya Ndani, Kipchumba Murkomen, ameagiza maafisa wa Polisi kuondoa mara moja watu wanaodaiwa kukalia ardhi kinyume cha sheria katika makazi ya Two Rivers Crescent na Imani, eneo la Mukuyu, Ruiru, Kaunti ya Kiambu.
Murkomen alitoa agizo hilo leo Jumatano, Novemba 11, 2026, baada ya kukutana na wawakilishi wa makazi hayo ili kusikiliza changamoto za kiusalama zinazohusiana na migogoro ya ardhi katika eneo hilo.
Alielekeza Huduma ya Kitaifa ya Polisi, NPS, kuhakikisha watu wote wanaokalia maeneo hayo kinyume cha sheria wanaondolewa.
Alionya kuwa mtu yeyote atakayebainika kutumia vibaya silaha, hata akiwa na leseni halali, atanyang’anywa silaha hizo kwa mujibu wa sheria na kufunguliwa mashtaka.
Waziri huyo pia alionya maafisa wa polisi dhidi ya kukwepa majukumu yao, akisema watakaobainika kushindwa kutekeleza wajibu wao katika kushughulikia mzozo huo watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Katika kuimarisha usalama katika eneo hilo lenye wakazi wengi, Murkomen alitangaza mipango ya kuongeza idadi ya maafisa wa polisi, kuanzisha doria za mara kwa mara katika makazi hayo mawili na kupatia Kituo cha Polisi cha Ruiru gari.
Waziri Murkomen alikuwa ameandamana na maafisa wakuu wa usalama, akiwemo Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Eliud Lagat, Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi wa Utawala Gilbert Masengeli na Mkurugenzi wa DCI Mohamed Amin.