Maeneo yote nchini kunufaika na maendeleo, asema Ruto

Amesema serikali yake inachukua hatua za kimakusudi kukabiliana na visa vya kutengwa, kupuuzwa na kiubaguzi vilivyofanywa miongo kadhaa iliyopita.  

Martin Mwanje
3 Min Read

Maeneo na jamii zote nchini zinatendewa sawa katika usambazaji na ugavi wa rasilimali za kitaifa.

Rais William Ruto amesema sera hii itasaidia kuangazia madhila ya kihistoria na kukuza umoja wa kitaifa.

Akizungumza mjini Keroka katika eneo bunge la Nyaribari Masaba, kaunti ya Kisii leo Jumatano, Rais Ruto alisema serikali yake inachukua hatua za kimakusudi kukabiliana na visa vya kutengwa, kupuuzwa na kiubaguzi vilivyofanywa miongo kadhaa iliyopita.

Aliyasema hayo wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Keroka-Ibacho-Kiamokama katika eneo bunge hilo.

Aliahidi kuwa hakuna sehemu ya Kenya itakayoachwa nyuma katika ajenda ya kitaifa ya maendeleo bila kujali sehemu hiyo iko wapi au kabila.

Rais aliongeza kuwa utawala wake umedhamiria kutokomeza ubaguzi, kufeli kwa sera, na upatikanaji usiokuwa wa usawa wa fursa ambazo kwa miaka mingi zilipatikana tu katika baadhi ya sehemu za nchi.

“Kwa miongo kadhaa, baadhi ya sehemu za nchi yetu zilimetengwa na kutopata rasilimali za kitaifa kwa usawa, hivyo kuwanyima raia fursa za kufikia uwezo wao kamili,” alilalama Ruto.

Lakini kupitia ajenda ya kimakusudi ya maendeleo yenye usawa ya – Usawa ni Sawa – Ruto alielezea kuwa utawala wake kwa sasa unasahihisha na kubatilisha ukosefu wa usawa wa kihistoria kwa kutekeleza mipango ya maendeleo, mmoja baada ya mwingine.

Alisema hatua hiyo itahakikisha hakuna sehemu inayoachwa nyuma kimaendeleo.

Aidha, aliwahakikishia wakazi wa kaunti ya Kisii kwamba serikali itatembea nao bega kwa bega kama inavyofanya katika sehemu zingine za nchi, ikibuni mazingira wezeshi kwa kila raia kufikia matamanio yake.

Wakati wa ziara hiyo, Ruto alizindua mradi wa uunganishaji umeme wa Last Mile katika eneo bunge la Nyaribari Masaba katika kaunti ya Kisii.

“Tayari tunaunganisha umeme kwenye nyumba 3,000 kwa kima cha shilingi milioni 150, kuwezesha kaya zaidi, kuboresha utoaji huduma na kupiga jeki biashara,” alisema Rais.

Kadhalika, alizindua Chuo cha Mafunzo ya Matibabu cha Kenya, KMTC katika eneo bunge la Nyaribari Chache.

Ni wakati huo ambapo alisema serikali inabadilisha sheria ya elimu ya juu ili kuhakikisha wanafunzi wote wa vyuo vikuu, vyuo vya kiufundi na KMTC wanapata ufadhili kamili kuanzia mwaka ujao.

“Sera hii itatoa fursa sawa na upatikanaji wa elimu bora kutimia,” alisema Ruto.

Rais amekamilisha ziara ya siku nne katika eneo la Kisii leo Jumatano ambapo alizindua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Share This Article