Koech atetea Afrika katika mazungumzo ya amani

Anaongoza ujumbe wa wabunge unaojumuisha Muchina Mwangi, Fredrick Ikana, Duncan Maina na Martin Owino.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Ulinzi, Ujasusi na Mahusiano ya Kigeni, Nelson Koech, ameungana na viongozi wa kimataifa katika kongamano la tisa la amani la Paris nchini Ufaransa.

Mazungumzo katika kongamano hilo yanajikita katika namna ya kusawazisha mahitaji ya usalama wa kitaifa na vipaumbele vya kijamii, kuimarisha usimamizi wa bunge katika mazingira ya usalama yanayobadilika, pamoja na kukuza ushirikiano wa kimataifa na baina ya mabunge.

Koech anaongoza ujumbe wa wabunge unaojumuisha Muchina Mwangi, Fredrick Ikana, Duncan Maina na Martin Owino.

Ujumbe huo umeshiriki mijadala inayolenga kuimarisha sauti ya Afrika katika mazungumzo ya usalama duniani, hususan katika kushughulikia migogoro, kuhimiza utulivu na kujenga amani endelevu barani Afrika.

Kongamano hilo pia linatoa fursa kwa viongozi wa mabunge kubadilishana mawazo kuhusu changamoto mpya za usalama duniani na nafasi ya taasisi za kutunga sheria katika kuhakikisha sera za usalama zinazingatia mahitaji ya wananchi huku zikilinda maslahi ya kitaifa.

Aidha, jukwaa hilo linalenga kuimarisha ushirikiano kati ya mabunge na washirika wa kimataifa katika kukabiliana na vitisho vya usalama vinavyovuka mipaka, kuzuia migogoro na kuendeleza kuishi kwa amani.

Share This Article