Tume ya filamu ya Kenya, KFC, imetangaza wito kwa watengenezaji filamu wa humu nchini, kuwasilisha kazi zao kwa ajili ya Tamasha ya Filamu ya Mashariki.
Tamasha hiyo almaarufu Mashariki African Film Festival, itafanyika jijini Kigali, nchini Rwanda, Novemba 23 hadi 29, 2026.
Katika taarifa iliyochapishwa na KFC, wabunifu na watengenezaji filamu wametakiwa kuwasilisha miradi yao ili kupata fursa ya kuionyesha, kukutana na wadau wa tasnia ya filamu na kutafuta ushirikiano mpya.
Tamasha hiyo pia itakuwa na jukwaa la Mashariki Market ambalo ni soko la filamu, kuanzia Novemba 27 hadi 29, likilenga kuwaunganisha wataalamu wa ubunifu na wadau mbalimbali wa sekta ya filamu.
Mwisho wa kuwasilisha miradi ni Novemba 15, 2026, huku wahusika wakihimizwa kuhakikisha wanawasilisha kazi zao kabla ya tarehe hiyo.
Fursa hiyo inalenga kuwapa wabunifu wa Afrika nafasi ya kuongeza mwonekano wa kazi zao, kupanua mitandao ya kitaaluma na kukutana na washirika watarajiwa katika tasnia ya filamu.
Tume ya Filamu Kenya imewahimiza watengenezaji filamu wenye miradi inayostahili kutumia fursa hiyo kuwasilisha maombi yao kabla ya muda wa mwisho.
Awamu hiyo ya 12 ya tamasha ya filamu ya Mashariki, itakuwa chini ya maudhui ya “Taswira za Ustahimilivu” yaani “Reels of Resilience”.
Filamu 80 kutoka zaidi ya nchi 30 zitaonyeshwa wakati wa tamasha hiyo, huku zikishindana katika vipengele vitano: Filamu Ndefu, Filamu Fupi, Filamu za Makala, Vipindi vya Televisheni na Filamu za Rwanda.