Evelyn Wanjiru atangaza awamu ya 8 ya Praise Atmosphere

Mwaka huu, itaandaliwa katika bustani ya Uhuru Gardens, Nairobi.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwimbaji wa nyimbo za injili nchini Kenya, Evelyn Wanjiru, ametangaza rasmi toleo la nane la tamasha ya Praise Atmosphere, litakaloandaliwa Disemba 5, 2026.

Tukio hilo huandaliwa kila mwaka na huwakutanisha waumini na wapenzi wa muziki wa injili kwa ajili ya sifa, ibada na ushirika. Mwaka huu, itaandaliwa katika bustani ya Uhuru Gardens, Nairobi.

Kupitia chapisho lake kwenye Instagram, Wanjiru ametajwa kuwa mhudumu mkuu wa ibada katika msimu wa nane wa tamasha hiyo, akiendeleza ushiriki wake katika hafla hiyo tangu ilipoanzishwa.

Toleo lijalo litafanyika chini ya kaulimbiu “Mbegu Imekua, Mwanzo Mpya Umefika. Tuote!”, inayosisitiza ukuaji, mageuzi na mwanzo mpya wakati tamasha hilo likiingia msimu wake wa nane.

Praise Atmosphere ilianzishwa kutokana na maono ya pamoja kati ya Wanjiru na mumewe, mtayarishaji maarufu wa muziki Agundabweni Akweyu.

Hafla hiyo isiyofungamana na dhehebu lolote la Kikristo inalenga kutoa jukwaa kwa watu kutoka madhehebu na mazingira mbalimbali ya Kikristo kukutana na kushiriki katika ibada, sifa na maombi.

Kwa miaka iliyopita, Praise Atmosphere imeendelea kuwa jukwaa la kuhamasisha imani, kuimarisha umoja wa waumini na kuwakutanisha watu kupitia muziki na huduma ya kiroho.

Waandaaji wamewahimiza mashabiki na waumini kujitokeza kushiriki katika msimu wa nane huku safari ya Praise Atmosphere ikiingia katika hatua mpya.

Share This Article