Viongozi wa dunia wakutana katika mkutano wa hali ya hewa Uturuki

Mkutano huo unafanyika wakati ambapo vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, kupanda kwa gharama za nishati na migogoro ya kiuchumi vimekuwa vikizikabili serikali mbalimbali duniani.

KBC Digital News
3 Min Read

Viongozi wa dunia wanatarajiwa kuanza kutoa hotuba zao mjini Antalya, Uturuki, Jumatano, Novemba 11, ikiwa ni siku ya tatu ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, unaojulikana kama COP31.

Mkutano huo ulioanza Jumatatu na unatarajiwa kuhitimishwa Novemba 20, unafanyika wakati ambapo vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, kupanda kwa gharama za nishati na migogoro ya kiuchumi vimekuwa vikizikabili serikali mbalimbali duniani.

Wawakilishi kutoka karibu nchi 200 wamekusanyika katika mkutano huo kujadili namna ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi, kuongeza matumizi ya umeme na kupunguza utegemezi wa dunia kwa nishati zinazotokana na mafuta ya kisukuku.

Iran pia inashiriki katika mkutano wa COP31. Vyombo vya habari vya kimataifa vimeripoti kuwepo kwa wajumbe wa ujumbe wa Iran mjini Antalya, lakini bado haijafahamika nani ataongoza ujumbe wa taifa hilo la Kiislamu na iwapo mwakilishi wake atahutubia mkutano wa viongozi.

Uturuki, ambayo ni mwenyeji wa mkutano huo, imependekeza kuongeza kiwango cha matumizi ya umeme katika matumizi ya jumla ya nishati duniani kutoka zaidi ya asilimia 20 ya sasa hadi asilimia 35 ifikapo mwaka 2035.

Mpango huo unalenga kupunguza utegemezi wa magari, viwanda na majengo kwa nishati zinazotokana na mafuta ya kisukuku.

Hata hivyo, wakosoaji wanasema kuongeza matumizi ya umeme pekee hakuhakikishi kupungua kwa uchafuzi wa mazingira, kwa kuwa pendekezo hilo halilazimishi umeme kuzalishwa kupitia vyanzo safi vya nishati kama vile jua na upepo.

Vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran pamoja na kukwama kwa usafirishaji wa mafuta kutoka Mashariki ya Kati vimeongeza gharama za nishati katika nchi nyingi na kuifanya usalama wa nishati kuwa kipaumbele tena kwa serikali mbalimbali.

Wakati huo huo, ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa imeonya kuwa dunia inaelekea kuvuka kiwango cha ongezeko la nyuzi joto 1.5 Selsiasi ikilinganishwa na viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda. Lengo hilo liliwekwa na nchi mbalimbali katika makubaliano ya hali ya hewa ya Paris ili kuepusha madhara makubwa zaidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Jumanne, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alizitaka serikali kuweka ratiba ya wazi ya kuachana na matumizi ya nishati za kisukuku, akisisitiza kuwa suala la kuhamia kwenye vyanzo safi vya nishati halipaswi tena kuonekana kuwa gumu kutekelezeka.

Taarifa ya BBC

Share This Article