Sudan imetangaza kuwa itaanza kuagiza tena majani chai kutoka Kenya baada ya kuondoa marufuku ya kuagiza bidhaa hiyo kutoka nchini humo.
Marufuku hiyo imetumika kwa kipindi cha miezi 20 iliyopita.
Nayo imeondolewa kufuatia mazungumzo yaliyofanyika awali kati ya Rais William Ruto na Waziri Mkuu wa Sudan Profesa Kamil Idris.
Mazungumzo hayo yalifanyika pembezoni mwa Mkutano wa Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali wa COMESA mjini Harare nchini Zimbabwe.
“Kenya inafurahia na kuthamini uamuzi huu, ambao unafungua tena soko muhimu kwa majani chai yetu, unarejesha fursa za wauzaji wa zao hilo nje ya nchi na kupiga jeki vyanzo vya mapato ya wakulima wetu na familia zao,” alisema Rais Ruto baada ya kutangazwa kuondolewa kwa marufuku hiyo.
“Hatua hii inaashiria kile ambacho mazungumzo na diplomasia yenye tija vinaweza vikafikia. Tunatazamia kuimarisha uhusiano wetu wa kidiplomasia, kupanua biashara na kufanya kazi pamoja kwa ajili ya amani, uthabiti na ustawi wa pamoja wa eneo letu.”