Jenerali Muhoozi amtaka Waziri Nameere amwombe msamaha

Haya yanafuatia kusambaa kwa video fupi inayomwonyesha Nameere akimwonya Jenerali huyo dhidi ya kuingilia wabunge wa chama tawala cha NRM.

Marion Bosire
2 Min Read
Justine Nameere, Waziri wa Nchi kuhusu Serikali za Mitaa, Uganda.

Mkuu wa Majeshi nchini Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba amempa Waziri Justine Nameere saa 72 kumwomba msamaha, la sivyo afutwe kazi na kupingwa katika kinyang’anyiro cha ubunge Masaka.

Jenerali Kainerugaba ametishia kufanya kampeni dhidi ya Waziri huyo wa Nchi kuhusu Serikali za Mitaa, huko Masaka huku muda aliompa wa kuomba radhi ukiendelea kuyoyoma.

Kainerugaba alisema jana kwamba wakazi wa Masaka wanamuunga mkono yeye na Rais Yoweri Museveni, lakini sio Nameere.

Tangazo lake limesababisha sintofahamu kuhusu mustakabali wa kisiasa wa Nameere katika Jiji la Masaka, ambako uchaguzi wake bado unapingwa.

Nameere alimshinda mgombea wa chama cha NUP, Rose Nalubowa, kufuatia zoezi la kuhesabu kura upya lililojaa utata.

Awali Tume ya Uchaguzi ilikuwa imemtangaza Nalubowa kuwa mshindi wa uchuguzi wa Januari 2026.

Vitisho vya Jenerali Muhoozi Kainerugaba vinatokana na video fupi inayosambaa ambayo inamwonyesha Nameere akimwonya Jenerali huyo dhidi ya kuingilia wabunge wa chama tawala cha NRM.

Hata hivyo, video ndefu ambayo haijahaririwa ilichapishwa na kuonyesha kwamba Nameere alikuwa akielekeza maneno yake kwa Katibu Mkuu wa PLU, Daudi Kabanda, na sio Jenerali Muhoozi.

Licha ya madai kwamba video hiyo ilinukuliwa nje ya muktadha au kuhaririwa na wapinzani wa kisiasa, Muhoozi alitoa makataa siku 7 awali na baadaye kupunguza hadi saa 72 kwa Waziri huyo kuomba msamaha hadharani, huku akitishia kumuondoa kwenye nafasi yake ya uwaziri iwapo atashindwa kutekeleza agizo hilo.

Share This Article