S2Kizzy asema hafai kufananishwa na yeyote Afrika Mashariki

Anasema hakuna hata mmoja aliye katika kiwango chake kwa kila kitu hasa miziki aliyozalisha kufikia sasa.

Marion Bosire
2 Min Read

Mtayarishaji maarufu wa muziki nchini Tanzania S2kizzy, amejigamba akisema kwamba hafai kufananishwa na mtayarishaji yeyote wa muziki Afrika Mashariki.

S2Kizzy ambaye jina lake halisi ni Salmin Kasimu Maengo, alitumia Insta Stories kusema hayo ambapo aliandika, “Naomba nisifananishwe na mtayarishaji yeyote yule hasa Afrika Mashariki.”

Kizzy ambaye pia hujiita Zombie, aliongeza kusema kwamba hakuna hata mmoja aliye katika kiwango chake kwa kila kitu hasa miziki aliyozalisha kufikia sasa.

“Ni kulikosea sana jina langu heshima. Nina hit mpaka nina hit tena mpaka ninashindana na mimi mwenyewe. kwa hivyo, tajeni watayarishaji wenu wengine lakini sio zombie.” alisema.

Huku hayo yakijiri, S2Kizzy ameahidi mashabiki zake kwamba anazindua albamu mpya mwezi ujao wa Oktoba, huku akiwahimiza wataje wasanii wanaotaka kuwasikia kwenye kazi hiyo ya sanaa.

S2kizzy amekuwa jina kubwa kwenye muziki wa Bongo Flava, baada ya kujifunza utayarishaji wa muziki akiwa shule ya bweni, kazi zake zinazofahamika zikijumuisha “Tetema” na “Amaboko” ambazo zilikuwa hits kubwa duniani zikiwahusisha Diamond Platnumz na Rayvanny mtawalia.

Hivi sasa, kionjo chake cha sauti cha “Zombie” kimebaki kuwa alama ya ubora wa nyimbo zinazoongoza chati.

Zaidi ya kubadili mwelekeo wa muziki wa sasa wa Tanzania, nguli huyu anaendelea kuvuka mipaka ya kikanda, akionyesha urithi wake kama mmoja wa magwiji wa muziki wenye ushawishi mkubwa zaidi Afrika Mashariki.

Share This Article