Wasomi wa sheria wahimizwa kuongeza ufahamu kuhusu sheria ya kugawa mali ya ndoa

Jaji Njoki Ndung'u anasema wanaweza kufanya hivyo kupitia kuwa marafiki wa mahakama, katika kesi zinazoendelea.

Marion Bosire
2 Min Read

Jaji wa Mahakama ya Juu nchini Kenya, Justice Njoki Ndung’u, amewataka wasomi wa sheria kushiriki kikamilifu zaidi katika maendeleo ya ufahamu kuhusu sheria ya mali za ndoa.

Kulingana naye, wasomi hao wanaweza kufanya hivyo kupitia kwa kuwa marafiki wa mahakama, katika kesi zinazosikilizwa mahakamani.

Jaji Ndung’u alitoa wito huo alipokuwa akitoa hotuba ya umma iliyopatiwa jina la “Division of Matrimonial Property upon Dissolution of Marriage in Kenya” katika Chuo Kikuu cha Strathmore.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wanafunzi na wahadhiri kutoka taasisi ya Strathmore pamoja na Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Nairobi.

Katika mhadhara huo, Jaji Ndung’u alieleza mabadiliko ya ufahamu kuhusu kugawanya mali ya ndoa, akizingatia hasa maamuzi muhimu yaliyotolewa na Mahakama ya Juu.

Pia alichunguza mielekeo mipya katika suala hilo, kama vile kuongezeka kwa utambuzi na matumizi ya mikataba ya kabla ya ndoa nchini Kenya.

Jaji Ndung’u alisisitiza kuwa wasomi wana nafasi muhimu katika kuunda na kuendeleza sheria, akiwahimiza kuchangia sio kupitia tafiti na maandishi ya kitaaluma pekee, bali pia kwa kushiriki moja kwa moja katika kesi kama marafiki wa mahakama.

Mhadhara huo ulifuatwa na majadiliano ambapo wanafunzi waliuliza maswali na kutoa mitazamo yao kuhusu suala hilo, hivyo kuimarisha mazungumzo kati ya Mahakama na jumuiya ya wasomi.

Share This Article