LSK yaandaa semina kuhusu ugatuzi Mombasa

Inalenga kuimarisha ujuzi wa kisheria kuhusu usimamizi wa serikali za kaunti na utekelezaji wa mfumo wa ugatuzi

Marion Bosire
1 Min Read

Chama cha Wanasheria nchini Kenya, LSK, kimeanzisha semina ya siku tatu kuhusu ugatuzi, inayolenga kuimarisha ujuzi wa kisheria kuhusu usimamizi wa serikali za kaunti na utekelezaji wa mfumo wa ugatuzi.

Rais wa LSK, Charles Kanjama, ambaye pia ni Wakili Mkuu, alifungua rasmi semina hiyo jijini Mombasa, kulingana na taarifa iliyochapishwa na chama hicho kwenye mitandao ya kijamii jana Jumatano.

Mafunzo hayo yameandaliwa kwa ushirikiano kati ya Kamati ya LSK ya Maendeleo Endelevu ya Kitaaluma na Kamati ya Kaunti na Serikali Zilizogatuliwa, inayoongozwa na mjumbe wa baraza la LSK, Faith Jappann.

Semina hiyo imewakutanisha maspika wa mabunge ya kaunti, mawakili wa kaunti na wataalamu wengine wa sheria. Majadiliano yanatarajiwa kujikita katika ugatuzi na masuala ya kisheria yanayohusiana na utendaji wa serikali za kaunti.

Miongoni mwa wazungumzaji ni Muthomi Thiankolu na Elisha Ongoya, wote Wakili Wakuu, Dkt. Kamotho Waiganjo mtaalamu wa utawala na sheria Conrad Bosire, pamoja na Brian Mutie, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Kiufundi katika Afisi ya Mdhibiti wa Bajeti.

Wengine ni Faraji Chipinde wa Kaunti ya Kilifi, Lucy Kibonei wa Kaunti ya Trans Nzoia na Dinah Katema wa Kaunti ya Taita Taveta.

Washiriki watatunukiwa alama nne za CPD kila mmoja baada ya kukamilisha mafunzo hayo.

Share This Article