Rais William Ruto ametangaza nyongeza ya mshahara kwa asilimia 36 kwa maafisa wa polisi wa cheo cha konstebo.
Nyongeza hiyo inakalimilisha awamu ya tatu ya nyongeza ya mishahara kwa polisi wa cheo cha konstebo ambacho ndicho kiwango cha kuanzia.
Ruto alisema haya Ijumaa aliposhuhudia hafla ya kufuzu kwa makurutu 3,000 wa Polisi wa Utawala katika Chuo cha Kutoa Mafunzo ya Polisi cha Embakasi, kaunti ya Nairobi.
Aliongeza kuwa mipango inaendelea ya kupanua mpango wa nyumba kwa maafisa wa polisi na kuboresha huduma za afya kwa polisi na jamaa zao 138,000 kupitia kwa huduma ya Usalama Cover.
Mshahara ambao haujaongezwa marupurupu kwa polisi wa konstebo umeongezwa kutoka shilingi 27,470 hadi shilingi 29,360.
Aidha, maafisa wa cheo cha koplo watapata nyongeza ya shilingi 1,890 kutoka shilingi 33,690 hadi 35,580 huku Masajini wa kiwango cha PG3 wakipata mshahara wa shilingi 46,380.