Nyota wa muziki wa Bongo Fleva nchini Tanzania, Mbosso, anatarajiwa kutumbuiza mashabiki zake nchini Kenya Novemba 8, 2026.
Mbosso ambaye jina lake halisi ni Mbwana Yusuph Kilungi, atakuwa mtumbuizaji mkuu wa tamasha iitwayo ‘The Warm Up Series’, siku hiyo ndani ya eneo la burudani la Al Capone, kwenye barabara ya Thika, mkabala na Garden City Mall.
Tamasha hiyo pia itawakutanisha wasanii mbalimbali wa Kenya, wakiwemo Iyanii, Bensoul, Njerae na Watendawili, ambao wanajulikana kwa mitindo tofauti ya muziki.
Mbosso, anayefahamika kwa nyimbo zake za mapenzi zenye hisia kali pamoja na vibao maarufu vya Bongo Flava, atakuwa miongoni mwa wasanii wanaotarajiwa kuvutia mashabiki katika hafla hiyo.
Mashabiki watapata fursa ya kufurahia muziki wake moja kwa moja jukwaani pamoja na burudani kutoka kwa wasanii wengine.
Kwa kuwakutanisha wasanii kutoka Tanzania na Kenya, tamasha ya The Warm Up Series inatarajiwa kuwapa mashabiki nafasi ya kufurahia ladha mbalimbali za muziki katika ukumbi mmoja.