Wasanii nchini Tanzania wana kina sababu ya kutabasamu baada ya shirika linalosimamia hakimiliki COSOTA kugawa mirabaha.
Diamond Platnumz na Alikiba ni miongoni mwa wanamuziki walionufaika zaidi na mgawo huo, huku Diamond akiongoza kwa kupata Shilingi milioni 12.2.
Katika mgawo huo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Alhamisi, Novemba 26, 2026, Diamond, ambaye jina lake halisi ni Nasib Abdul, aliibuka kinara katika kundi la wasanii wa muziki.
Mpinzani wake wa muda mrefu katika Bongo Fleva, Ali Saleh maarufu Alikiba, alijipatia Shilingi milioni 7.3, huku Kwaya ya Mtakatifu Cecilia kutoka Arusha ikishika nafasi ya tatu kwa kupata Shilingi milioni 6.8.
Mgawo huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha wasanii, watunzi na wadau wengine wa ubunifu wanalipwa kutokana na matumizi ya kazi zao.
Mbali na wanamuziki, malipo hayo yalihusisha pia wadau wa filamu, sanaa za ufundi, maonesho na uandishi.
Hatua hiyo inaendelea kuibua matumaini kuhusu ukuaji wa mfumo wa mirabaha nchini, huku uwazi katika ukusanyaji na ugawaji wa mapato ukiendelea kuwa suala muhimu kwa wadau wa tasnia ya ubunifu.