Mahakama kuu yaruhusu KIM kuendeleza shughuli

Mahakama Kuu ya Milimani ilitupilia mbali uamuzi wa TVETA wa Aprili 20, 2026, wa kufuta ithibati na idhini ya KIM.

Marion Bosire
2 Min Read
Dr. Muriithi Ndegwa, Afisa Mkuu Mtendaji, KIM

Mahakama Kuu jijini Nairobi imebatilisha agizo la Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Ustadi, TVETA, la kufunga matawi yote ya Taasisi ya Mafunzo ya Usimamizi ya Kenya, KIM, nchini.

Katika uamuzi uliotolewa Novemba 24, 2026, Mahakama Kuu ya Milimani ilitupilia mbali uamuzi wa TVETA wa Aprili 20, 2026, wa kufuta ithibati na idhini ya KIM.

Mahakama ilisema mamlaka hiyo haikufuata taratibu za kisheria zilizowekwa chini ya vifungu vya 36 na 37 vya Sheria ya TVET kabla ya kuchukua hatua dhidi ya taasisi hiyo.

Baada ya uamuzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa KIM, Dkt. Muriithi Ndegwa, alihakikishia wanafunzi, wafanyakazi na wadau kuwa shughuli zote za masomo zitaendelea bila kukatizwa, zikiwemo mihadhara, mitihani na tathmini.

Mzozo huo ulianza Aprili mwaka huu, TVETA ilipoishutumu KIM kwa kutoa kozi zisizoidhinishwa, kutunuku vyeti nje ya mamlaka yake na kuajiri wakufunzi wasio na leseni halali.

Mamlaka hiyo pia ilitangaza kuwa vyeti na stashahada zilizotolewa na KIM tangu mwaka 2018 hazitatambuliwa kwa ajira wala kujiendeleza kielimu, hali iliyozua wasiwasi miongoni mwa wahitimu na wanafunzi.

Wizara ya Elimu baadaye ililihakikishia Bunge kuwa sifa hizo zilikuwa zikitathminiwa.

Uamuzi wa mahakama unamaanisha kwamba agizo la kufungwa kwa KIM limebatilishwa, hivyo taasisi hiyo inaweza kuendelea na shughuli zake za kawaida.

Share This Article