Mpango wa pensheni wa wasanii wazinduliwa

MSANII Savings and Pension Plan ulizinduliwa leo ukiwapa wasanii fursa ya kuweka akiba ambapo michango inaanzia shilingi elfu 1 pekee.

Marion Bosire
1 Min Read

Tume ya Filamu Nchini Kenya, KFC, kwa ushirikiano na Hazina ya Pensheni ya Serikali za Mitaa, LAPFUND, imezindua mpango mpya wa akiba na pensheni unaolenga wataalamu katika sekta ya ubunifu nchini Kenya.

Mpango huo unaojulikana kama “MSANII Savings and Pension Plan”, ulizinduliwa leo Ijumaa, Novemba 27, 2026, katika Hoteli ya Nairobi Safari Club, ukiwapa wasanii fursa ya kuweka akiba kwa ajili ya usalama wao wa kifedha wa baadaye. Michango inaanzia shilingi elfu 1 pekee.

Mpango huo unawalenga wadau katika nyanja mbalimbali za ubunifu, zikiwemo filamu, muziki, sanaa za maonyesho, sanaa za picha na utengenezaji wa maudhui ya kidijitali.

Kwa mujibu wa Tume ya Filamu Kenya, mpango huo unalenga kukabiliana na changamoto za kifedha zinazowakabili wasanii wengi wanaofanya kazi kwa mikataba ya muda mfupi, kujitegemea au miradi yenye kipato kisicho na uhakika.

Kupitia ushirikiano huo, KFC na LAPFUND zinalenga kuimarisha utamaduni wa kuweka akiba na kupanua upatikanaji wa mipango rasmi ya pensheni na ulinzi wa kijamii kwa wadau wa sekta ya ubunifu.

Uzinduzi huo ni hatua muhimu katika kuimarisha usalama wa kifedha wa wasanii wanapostaafu.

Share This Article