Wasanii na wadau mbalimbali wa tasnia ya burudani, mitindo na biashara nchini Tanzania wameanza kupokea mialiko ya kuhudhuria hafla maalumu ya ‘Heshima kwa Mkubwa’.
Shughuli hiyo inalenga kumuenzi na kumchangia meneja mkongwe wa wanamuziki nchini Tanzania, Said Fella maarufu kama Mkubwa Fella.
Hafla hiyo inatarajiwa kufanyika Jumapili, Novemba 29, 2026, katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, kuanzia saa 4 asubuhi.
Miongoni mwa walioalikwa ni Alikiba, Marioo, Juma Nature, Inspector Haroun, Ambwene Yessayah (AY), Jokate Mwegelo, Flaviana Matata, Fred Vunjabei, Dominic Mmasi wa Room of Jeans na Jessica Kikumbi wa Kitambaa Cheupe Investment.
Tukio hilo limeandaliwa kwa ushirikiano wa Jumuiya ya Wanahabari wa Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA) na TMK Wanaume Family, likiwa na kaulimbiu ya “Kusherehekea Urithi wa Mkubwa Fella”.
Mbali na kutambua mchango wa Fella katika kukuza muziki wa Bongo Fleva, hafla hiyo pia inalenga kuchangisha fedha za kumsaidia kukabiliana na changamoto za kiafya na kimaisha.
Mkubwa Fella anayejulikana sana kwa usimamizi wa iliyokuwa bendi ya Yamoto na usimamizi wa Diamond Platnumz, amekuwa akikumbwa na matatizo ya kiafya tangu mwisho wa mwaka 2024.
Wasanii walishirikiana wakati huo katika kuhakikisha wanagharamia matibabu yake akiwemo Diamond Platnumz na sasa wameamua kumchangia fedha zaidi huku wakimsherehekea yeye pamoja na mchango wake katika tasnia.