Mwimbaji wa nyimbo za injili nchini Kenya, Dkt. Sarah K, amejishindia tuzo mbili katika tuzo za nyimbo za injili Afrika Mashariki yaani East Africa Gospel Music Awards.
Hafla ya kugawa tuzo hizo iliandaliwa usiku wa Jumamosi Novemba 14, 2026, katika ukumbi wa Superdome huko Masaki, jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania.
Sarah K alitangazwa mshindi wa tuzo za “Msanii Bora wa nyimbo za Sifa” yaani “Praise Artist of the Year” na “Mwanamuziki Bora wa Kutumbuiza Moja kwa Moja” yaani “Best Live Performer of the Year” katika hafla hiyo.
Akifurahikia ushindi huo, Sarah K alisema kwamba Utukufu wote, heshima na sifa zimrudie Mungu! Kwani Kutambuliwa kwake ni ukumbusho kwamba kila kipawa, kila fursa na kila jukwaa hutoka kwa Mungu.
“Ni kwa neema yake tunasimama, kwa nguvu zake tunamtumikia na kupitia wema wake tunaendelea kufanya yale tunayoyafanya” aliendelea kusema huku akimalizia kifungu cha Biblia, Zaburi 115:1.
Toleo la pili la tuzo hizo za kila mwaka liliwakutanisha waimbaji wa nyimbo za injili, kwaya, watayarishaji wa muziki na wabunifu wengine kutoka mataifa ya Afrika Mashariki kwa lengo la kutambua mchango wao katika muziki wa injili.
Ushindi huo wa tuzo mbili unaongeza hadhi ya Sarah K katika tasnia ya muziki wa injili Afrika Mashariki.