Mwanamuziki wa Uganda, Spice Diana, amewakosoa wasanii wenzake wanaoendesha vipindi vya mtandaoni almaarufu podcast zinazojikita katika umbea.
Mrembo huyo anahoji manufaa ya vipindi hivyo akisema hataki kutumia muda wake kwenye mijadala isiyoongeza thamani katika nembo yake kama mwanamuziki.
Spice Diana amesema hana nia ya kuiga mtindo huo unaozidi kushika kasi miongoni mwa wasanii wa Uganda, akifichua kuwa anaandaa mradi tofauti utakaotoa mwelekeo mpya katika tasnia ya burudani.
Wasanii kadhaa wa Uganda wakiwemo Bruno K, Sheebah na Kalifah AgaNaga wameingia katika ulimwengu wa podcast kupitia majukwaa kama YouTube na TikTok, ambako hujadili masuala ya burudani, kutangaza muziki na kuzungumzia maisha ya mastaa, ikiwemo umbea.
Akizungumza katika mahojiano, Spice Diana alisema mradi anaoandaa hautafanana na podcast za kawaida zinazotumia viti, vipaza sauti na mahojiano.
Alisisitiza kuwa hataki kujihusisha na mijadala ya umbea bila kupata manufaa yoyote ya kikazi au kibiashara.
Ingawa hakufichua maelezo zaidi kuhusu mradi huo, msanii huyo ambaye anatarajiwa kufanya tamasha mwaka ujao alisema anataka kuja na ubunifu tofauti badala ya kufuata mtindo ambao tayari umezoeleka miongoni mwa wasanii wengine.