Msanii wa muziki nchini Kenya na mtaalamu wa masuala ya rasilimali watu, Akothee, amemwomba Rais William Ruto kuingilia kati na kuharakisha ujenzi wa Daraja la Migori lililoporomoka.
Akothee anasema wakazi wamekuwa wakiteseka kwa karibu mwaka mmoja.
Katika barua ya wazi aliyochapisha kwenye Facebook, Akothee, ambaye jina lake halisi ni Esther Akoth Kokeyo, alisema kuporomoka kwa daraja hilo kumeathiri biashara, maisha ya wakazi na upatikanaji wa huduma muhimu, huku wanafunzi, wafanyabiashara, wagonjwa na wasafiri wakikumbwa na changamoto.
Alielezea hali hiyo kuwa tishio kwa usalama wa wananchi, akidai kuwa wanaotembea kwa miguu kwenye njia zisizo rasmi wanakabiliwa na visa vya uporaji.
Akothee pia alisimulia jinsi aliamka saa 10 alfajiri kusafiri na babake ambaye ni mgonjwa kuelekea Nairobi kupata matibabu, akijaribu kuepuka msongamano wa magari unaosababishwa na kufungwa kwa daraja hilo.
Aidha, alielezea wasiwasi kuhusu wanafunzi ambao wanakabiliwa na changamoto za kufika shuleni, muhula mwingine wa masomo ukikaribia.
Huku akipongeza miradi ya maendeleo ya serikali, Akothee alimtaka Ruto kuelekeza mamlaka husika kufuatilia maendeleo ya kazi zinazotekelezwa na Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu na kuharakisha ujenzi wa daraja hilo.
Alisema kurejeshwa kwa daraja hilo kutawezesha wakazi kufikia shule, hospitali, masoko na fursa za kiuchumi kwa urahisi.