Rais Milei amkaribisha Papa Leo Argentina

Argentina ni kituo cha pili katika ziara ya siku 12 ya Papa Leo huko Amerika Kusini, baada ya kuzuru Uruguay kwa siku tatu.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais wa Argentina, Javier Milei, amemkaribisha Papa Leo XIV jijini Buenos Aires katika ziara ya kwanza ya kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini humo baada ya takriban miaka 40.

Milei, akiandamana na dadake ambaye pia ni Katibu wa Rais, Karina Milei, alimpokea Papa katika Uwanja wa Ndege wa Jorge Newbery jana Jumapili kabla ya kuhudhuria hafla rasmi ya kumkaribisha katika Uwanja wa Plaza San Martín.

Katika hotuba yake ya kwanza nchini Argentina, Papa Leo alizitaka mamlaka kutanguliza ustawi wa wananchi kabla ya maslahi ya kiuchumi, akitoa ujumbe ulioonekana kupinga sera za uchumi huria za Milei.

“Uchumi unapaswa kumhudumia mwanadamu, wala si mwanadamu kuutumikia uchumi,” alisema Papa, akihimiza uwepo wa sera zinazowasaidia wasio na ajira, wastaafu na familia zinazokabiliwa na changamoto za kifedha.

Papa huyo pia alihimiza uwekezaji katika elimu na mafunzo ya ufundi, akionya kuwa vijana hawapaswi kulazimika kuondoka nchi yao ili kutimiza ndoto zao.

Argentina ni kituo cha pili katika ziara ya siku 12 ya Papa Leo huko Amerika Kusini, baada ya kuzuru Uruguay kwa siku tatu.

Akiwa Argentina, anatarajiwa kuzuru gereza na kuongoza misa katika miji ya Buenos Aires, Luján na Córdoba kabla ya kuelekea Peru Jumatano.

Ziara hiyo inafanyika wakati kuna mvutano kati ya serikali ya Milei na Kanisa Katoliki kuhusu hatua za kubana matumizi ya serikali, ikiwemo kupunguza matumizi ya umma na ruzuku.

Share This Article