Shirika linalohusika na hakimiliki nchini Kenya, KAMP, litafanya Mkutano Mkuu wa Mwaka, AGM, Jumatano, Oktoba 28, 2026, katika Chuo Kikuu cha Daystar, bewa la barabara ya Valley, Nairobi.
Mkutano huo, unaotarajiwa kuanza saa 4:00 asubuhi, utawakutanisha wanachama kujadili masuala muhimu yanayohusu shughuli na uendeshaji wa kampuni.
Kulingana na notisi iliyotolewa na Katibu wa Kampuni Oktoba 6, wanachama wataanza kwa kuthibitisha uwepo wa akidi kabla ya kuendelea na shughuli za kawaida.
Ajenda hiyo inajumuisha kuthibitisha kumbukumbu za Mkutano Mkuu wa Mwaka uliofanyika Desemba 17, 2025, kujadili ripoti ya Mwenyekiti anayemaliza muda wake kuhusu shughuli za Bodi kwa kipindi kilichoishia Septemba 30, 2026, pamoja na ripoti ya wakaguzi kuhusu taarifa za kifedha za kampuni kwa mwaka ulioishia Desemba 31, 2025.
Wanachama pia watajadili uteuzi wa wakaguzi wa kampuni na kuidhinisha Bodi ya Wakurugenzi kuamua malipo yao.
Jambo muhimu kwenye ajenda litakuwa uchaguzi wa Bodi ya Wakurugenzi kwa mujibu wa Mkataba na Kanuni za Kampuni.
Wanachama wanaotaka kuwasilisha masuala mengine wanatakiwa kuyawasilisha kwa Sekretarieti kabla ya Oktoba 15, 2026.
Wasioweza kuhudhuria wanaweza kumteua mwakilishi, huku fomu zilizojazwa zikitarajiwa kuwasilishwa pia kabla ya Oktoba 15.