Msanii wa R&B kutoka Marekani na mshindi wa tuzo tatu za Grammy, Ne-Yo, anatarajiwa kurejea Kenya baada ya miaka 11 kwa ajili ya tamasha maalum ya Siku Kuu ya Mashujaa itakayofanyika Nairobi Oktoba 20, 2026.
Nyota huyo ataongoza tamasha ya “One Night Only: Brunch Edition”, itakayofanyika katika Uwanja wa Michezo wa Ulinzi kuanzia saa 9 alasiri hadi saa 11 jioni.
Bendi ya maonyesho kutoka Uingereza ya Sol & The Gang, pia itatumbuiza katika hafla hiyo iliyoandaliwa na Fenon Premium Productions na Radio Africa Group kwa ushirikiano na Pernod Ricard.
Tamasha ya mwaka huu itakuwa katika mfumo wa chakula cha mchana, tofauti na matoleo yaliyopita. Mwaka jana, mpiga saxophone wa Marekani Kenny G aliongoza tamasha hiyo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta, KICC.
Ne-Yo, ambaye jina lake halisi ni Shaffer Chimere Smith, alitembelea Kenya mara ya mwisho Agosti 2015 wakati wa msimu wa tatu wa Coke Studio Africa.
Akiwa Nairobi, alirekodi wimbo “Marry You” pamoja na msanii wa Tanzania Diamond Platnumz, ambao ulipata umaarufu kote Afrika Mashariki.
Maonyesho yake Nairobi ni sehemu ya ziara yake barani Afrika, inayojumuisha pia Cape Town Oktoba 17 na Pretoria Oktoba 18.
Ne-Yo alipata umaarufu duniani kupitia albamu yake ya kwanza ya mwaka 2006, “In My Own Words”, iliyokuwa na kibao ‘So Sick’. Pia anajulikana kwa kuandika nyimbo maarufu, ikiwemo ‘Irreplaceable’ ya Beyoncé.