DPP ahimiza kuharakishwa kwa michakato ya kutafuta haki

Amesisitiza umuhimu wa kufupisha muda kati ya kuripotiwa kwa makosa ya jinai, uchunguzi, kufunguliwa kwa mashtaka na kutolewa kwa maamuzi ya mwisho ya mahakama.

Marion Bosire
2 Min Read
Jacinta Nyamosi, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, DPP ametoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya taasisi za haki na kuhusisha waendesha mashtaka mapema katika uchunguzi ili kupunguza kucheleweshwa kwa kesi mahakamani.

Wito huo umetolewa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma na Mkuu wa Idara ya Makosa ya Kawaida na Yanayohusiana nayo, Jacinta Nyamosi, aliyemwakilisha DPP katika uzinduzi wa Mpango wa Kimkakati wa mwaka 2026 hadi 2030 wa Baraza la Kitaifa la Usimamizi wa Haki, NCAJ.

Nyamosi alisisitiza umuhimu wa kufupisha muda kati ya kuripotiwa kwa makosa ya jinai, uchunguzi, kufunguliwa kwa mashtaka na kutolewa kwa maamuzi ya mwisho ya mahakama.

Alisema kuwahusisha waendesha mashtaka katika hatua za awali za uchunguzi kunawawezesha wachunguzi kukusanya ushahidi unaofaa, kuziba mapengo ya ushahidi na kuandaa kesi imara zaidi, hatua inayoweza kupunguza ucheleweshaji na kuongeza ufanisi katika mfumo wa haki.

Pia alihimiza kurahisishwa kwa taratibu za taasisi na kuimarishwa kwa uratibu kati ya mashirika ya sekta ya haki ili kuboresha utoaji wa huduma.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Jaji Mkuu Martha Koome, Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Muthomi Njuki, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai Amin Mohamed Ibrahim na Msajili Mkuu wa Mahakama Winfridah Boyani Mokaya, miongoni mwa wadau wengine.

Mpango huo wa miaka mitano unalenga kuimarisha uratibu na kuboresha utoaji wa haki kupitia ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali za sekta hiyo.

Share This Article