Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, amesema hakuna Mkenya atabaguliwa katika utoaji wa vitambulisho vya taifa.
Akizungumza katika kaunti ya Trans Nzoia, Murkomen alithibitisha kuwa serikali imepeleka huduma za utoaji vitambulisho karibu na wananchi, pamoja na kuondoa mchakato wa uchunguzi zaidi kwa jamii zinaoishi mipakani.
Waziri huyo aliwakashifu baadhi ya wanasiasa wanaopinga utoaji wa vitambulisho kwa Wakenya walio nje ya taifa hili, akidokeza kwamba serikali ya Kenya Kwanza haitambagua raia yeyote.
“Wakenya wote wakiwemo wale wanaishi katika mataifa jirani, wana haki ya kujisajili kuwa wapiga kura. Na ndio maana Kenya ina idara ya mambo ya ughaibuni, inayokusudiwa kuwasaidia Wakenya wanaoishi nje ya nchi,” alisema Murkomen.
Waziri huyo aliyasema hayo alipokuwa akikagua miradi ya maendeleo, hali ya usalama na utoaji huduma katika kaunti ya Trans Nzoia.
Alitoa wito kwa Wakenya kuchukua fursa ya mageuzi katika huduma ya usajili wa watu, kutuma maombi ya kuchukua vitambulisho,ili washiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.