Ruto: Wanaotaka kumtapeli Dangote wataambulia patupu

Mwekezaji huyo bilionea kutoka Nigeria anapania kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta katika kaunti ya Lamu kwa kima cha shilingi bilioni 2.2.

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais William Ruto ameapa kumlinda Aliko Dangote dhidi ya matapeli wanaokusudia kumhangaisha kutokana na matakwa yasiyokuwa na msingi na kuwasilisha kesi mahakamani.

Mwekezaji huyo bilionea kutoka Nigeria anapania kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta katika kaunti ya Lamu kwa kima cha shilingi bilioni 2.2.

Ujenzi wa kiwanda hicho unatarajiwa kuchukua kipindi cha takriban miaka mitatu.

Ruto amesema kundi la wanasiasa matapeli lilipanga njama ya kumhangaisha mfanyabiasha huyo, akionya kuwa utawala wake hautaruhusu maslahi ya kibinafsi kuhujumu uwekezaji mkubwa kama huo nchini.

Akizungumza katika Chuo cha Mafunzo ya Walimu cha Shanzu katika eneo bunge la Kisauni leo Alhamisi, Ruto aliapa kuwa kamwe hatakubali watu ambao awali walihujumu juhudi za Dangote kujenga kiwanda cha kutengeneza saruji nchini kuhujumu uwekezaji huu mpya

“Jana, nilisikia Mr Empty of Shiny Things akiulizia makubaliano ya kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote. Ametumwa na mfadhili wake kuuliza makubaliano hayo,” alisema Rais Ruto.

“Unafahamu taratibu za kufuata za serikali na bunge katika kuuliza taarifa kama hiyo. Lakini najua sababu halisi ya kuulizia makubaliano hayo ni ili umpelekee mfadhili wako kumtapeli Bw. Dangote – kama ulivyofanya awali.”

Rais Ruto aliyasema hayo siku moja baada ya kuzindua ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta katika kaunti ya Lamu kwenye hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Rais wa Uganda Yoweri Museveni.

Serikali inasema kiwanda hicho kitakuwa na manufaa ya kiuchumi siyo tu kwa nchi hii bali eneo zima la Afrika Mashariki.

Mathalan, kiwanda hicho kinatarajiwa kubuni nafasi za ajira zipatazo 50,000.

Share This Article