Wawakilishi wa vyama vya kisiasa kutoka Nyanza na Magharibi mwa Kenya wameeleza wasiwasi kuhusu kanuni za uchaguzi na uteuzi wa wagombea ndani ya vyama.
Wasiwasi wao unahusu jinsi kanuni hizo zinavyoathiri wanawake, vijana na walemavu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.
Wawakilishi hao walikutana Kisumu jana Jumatano katika mkutano ulioandaliwa na shirika la mawakili wa kike nchini FIDA-Kenya kujadili katiba na kanuni za uteuzi za vyama kabla ya kuwasilishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa.
Majadiliano yalilenga kubaini iwapo michakato ya uteuzi inatoa fursa sawa kwa makundi yaliyotengwa na namna kanuni ya kikatiba ya thuluthi mbili ya jinsia inaweza kutekelezwa ili kuwapa wanawake wanaotaka kugombea nyadhifa za kisiasa fursa halisi.
Washiriki pia walitaja unyanyasaji wa kingono, vitisho na ukatili wa kijinsia kuwa miongoni mwa vikwazo vikuu vinavyokabili wanawake katika siasa.
Mwanamke mmoja anayelenga kugombea wadhifa wa mwakilishi wa wadi ya Nyakach alieleza jinsi mpinzani wake alijaribu kumtafutia mume, akitumaini kwamba angeacha azma yake ya kisiasa.
Mkutano huo pia ulijadili upatikanaji wa rasilimali za kisiasa, likiweno suala la iwapo fedha kutoka Hazina ya Vyama vya Kisiasa huwafikia wanachama mashinani na kunufaisha wanawake, vijana na walemavu.
Watetezi wa walemavu walitoa wito wa kutambuliwa zaidi kwa walezi, wakisema wanawake wenye ulemavu hukabiliwa na vikwazo vingi.
FIDA-Kenya ilisema mapitio hayo yanalenga kuimarisha ushiriki wa kisiasa unaojumuisha wote, wenye uwazi na unaozingatia usawa wa kijinsia kuelekea 2027.