Mshawishi wa mitandao ya kijamii nchini Kenya Alvan Love amefichua kuwa anaishi na tatizo adimu la macho ambalo limeathiri kwa kiasi kikubwa uwezo wake wa kuona.
Akizungumza katika kongamano la mwaka 2026 la Taasisi ya Elimu Spesheli ya Kenya, KISE, Alvan alisema ana tatizo la macho linalofahamika kama keratoconus, hali inayobadilisha umbo la konea na kuathiri uwezo wa mtu kuona kwa uwazi.
Mshawishi huyo alisema miwani ya kawaida haiwezi tena kumsaidia kurekebisha uwezo wake wa kuona, hivyo amelazimika kutumia lenzi maalum za macho za ‘hard gas-permeable’ ili kumsaidia kuona.
Alieleza kuwa lenzi hizo maalum huagizwa kutoka nje ya nchi na zinaweza kuchukua hadi mwezi mmoja kufika, huku gharama yake ikiwa kubwa.
Alvan, anayejulikana kwa maudhui yake ya kuchekesha mtandaoni, alisema uzoefu wake umeimarisha shauku yake katika haki za kijamii, ujumuishaji na utawala bora.
Alihimiza Wakenya kubadili mtazamo wao kuhusu ulemavu, akisema vikwazo mara nyingi vinasababishwa na mazingira badala ya mtu mwenyewe.
“Ulemavu haupaswi kamwe kumaanisha kutoweza,” alisema, akitoa wito wa uwekezaji zaidi katika teknolojia saidizi, ubunifu na elimu jumuishi.
Alvan pia aliahidi kutumia majukwaa yake ya mitandao ya kijamii kuhamasisha ujumuishaji wa walemavu katika jamii.