Zuchu, Harmonize na S2kizzy waongoza Tanzania Charts Septemba

Tanzania Charts ni jukwaa la mtandaoni hususan Instagram lilalotumiwa kushindanisha wasanii katika vitengo mbali mbali.

Marion Bosire
2 Min Read

Nyota wa muziki wa Tanzania, Zuchu na Harmonize, pamoja na mtayarishaji wa muziki S2kizzy, wameibuka washindi katika vipengele vyao kwa mwezi Septemba 2026, kwenye Tanzania Charts.

Tanzania Charts ni jukwaa la mtandaoni hususan Instagram lilalotumiwa kushindanisha wasanii katika vitengo mbali mbali.

Zuchu alitawazwa Msanii Bora wa Kike wa Septemba 2026 baada ya kupata kura 82,000 kutoka kwa mashabiki waliopiga kura mtandaoni.

Ushindi huo unaonyesha kuendelea kuungwa mkono kwa mwimbaji huyo, ambaye amekuwa na nafasi muhimu katika tasnia ya muziki wa Bongo Flava nchini Tanzania.

Kwa upande wake, Harmonize alishinda tuzo ya Msanii Bora wa Bongo Flava wa Mwezi Septemba, huku Tanzania Charts ikimpongeza kwa ushindi huo.

Jukwaa hilo lilisema ushindi wake umetokana na mashabiki waliopiga kura na kuonyesha kuunga mkono muziki wake, likieleza kuwa mafanikio hayo yanaakisi uhusiano wa karibu kati ya wasanii na mashabiki wao.

Mtayarishaji wa muziki S2kizzy naye alitambuliwa kama Mtayarishaji Bora wa Muziki wa Mwezi Septemba kutokana na ubunifu wake, kipaji na mchango wake katika tasnia ya muziki.

Katika machapisho tofauti kwenye Instagram, Tanzania Charts ilitoa heshima kwa washindi hao watatu na kushukuru waliopiga kura.

Jukwaa hilo, ambalo linasema chati zake zinatokana na kura halisi za mashabiki, lilieleza kuwa tuzo hizo ziliwezekana kutokana na ushiriki wa umma.

Share This Article