Mariam Abdulmagid ndiye sura ya Sabala Fest@20

Alishinda kinyang’anyiro cha kumtafuta nyota wa kitamaduni wa jamii ya Nubia mwaka 2026.

Marion Bosire
1 Min Read

Mariam Abdulmagid ameteuliwa kuwa sura na balozi wa tamasha ya Sabala Fest mwaka 2026, huku tamasha ikiadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake.

Mariam aliye na umri wa miaka 23 alishinda kinyang’anyiro cha kumtafuta nyota wa kitamaduni wa jamii ya Nubia mwaka 2026, baada ya mchakato wa ushindani uliowakutanisha wanawake vijana wa jamii ya Wanubi kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa waandaaji, Mariam alijitokeza katika mchakato wa uteuzi kutokana na haiba yake, uwezo wa kiakili na uhusiano wake mkubwa na utamaduni na urithi wa Wanubi.

Kama nyota mpya wa utamaduni wa Wanubi, Mariam atawakilisha katika Sabala Fest 2026, ambayo itaadhimisha miongo miwili ya kusherehekea utamaduni, urithi na ubora wa Afrika.

Mbali na jukumu lake la kitamaduni, Mariam ni mtaalamu wa huduma za mapokezi na mjasiriamali anayejihusisha na biashara ya kuoka bidhaa za chakula na utengenezaji wa sabuni.

Uteuzi wake unajiri wakati maandalizi ya toleo la 20 la Sabala Fest yakipamba mshawasha. Tamasha hiyo imetajwa kuwa miongoni mwa tamasha kubwa za kitamaduni barani Afrika.

Waandaaji wanatarajiwa kutangaza rasmi tarehe na eneo litakalofanyika Sabala Fest@20 Jumatatu, Septemba 21, saa 10:00 asubuhi.

Kwa Mariam kuchukua nafasi ya balozi wa utamaduni, safari kuelekea Sabala Fest@20 imeanza rasmi.

Share This Article